Na Mwandishi Wetu, Manyara
Ajali mbaya ya barabarani imesababisha vifo vya watu watatu, wakiwemo mume na mke waliokuwa pembezoni mwa barabara, baada ya bodaboda aliyekuwa mwendokasi kuacha njia na kuwagonga katika Kijiji cha Matufa, kata ya Magugu, wilayani Babati mkoani Manyara.
Kwa mujibu wa viongozi wa kijiji hicho, akiwemo Deogras Ngalawa aliyetoa taarifa kwa niaba ya mwenyekiti wa kijiji, ajali hiyo imetokea wakati bodaboda hao wakishindana katika barabara kuu ya Babati-Arusha.
"Hawa Vijana ikifika jioni huwa wanakutana kushindana mbio na kuchanga hela kumpa mshindi, tunaomba jeshi la polisi lichukue hatua" alisema Ngalawa
Ngalawa ameongeza kuwa ni tabia ambayo imekemewa mara nyingi lakini vijana hao hawataki kusikia.
Imeelezwa kuwa dereva wa bodaboda huyo alipoteza mwelekeo kutokana na kasi kubwa, na kusababisha mauti hayo.
Akizungumza baada ya kupata taarifa za tukio hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, ametoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao, akiwataka madereva wa bodaboda kuacha kufanya mzaha barabarani na kutii sheria za usalama barabarani.
“Ni jambo la kusikitisha sana. Kila mmoja anatakiwa kuthamini uhai wake na wa wengine. Mashindano yasiyo rasmi na mwendokasi ni hatari. Serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha madereva wote wanazingatia kanuni za usalama,” alisema Sillo.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati Vijijini, Jackson Haibei, ambaye naye alifika Kituo cha afya Magugu aliwafariji wafiwa na kuwahakikishia kuwa chama na serikali wapo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Miili ya marehemu ilihifadhiwa katika Kituo cha afya Magugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.



0 Comments