Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali, ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua Semina ya Maafisa Usafirishaji (Bodaboda) na Mawakala wa Huduma za Fedha wa Wilaya hiyo iliyofanyika Oktoba 22, 2025
..............................................
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida imetoa semina kwa maafisa usafirishaji (BODABODA) na Mawakala wa Huduma za Kifedha kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu.
Akifungua semina hiyo mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Moses Machali ambaye alikuwa mgeni rasmi aliipongeza TAKUKURU kwa hatua ya kufanya semina hiyo kwa kundi hilo ambalo ni la muhimu katika jamii.
“Maafisa hawa usafirishaji ni kundi mtambuka na la muhimu
kwani linajishughulisha na kazi ambayo inaigusa jamii kwa kiasi kikubwa
kutokana na kurahisisha maisha ya watu katika suala zima la uchukuzi wa abiria
na mizigo,” alisema Machali.
Machali alisema maafisa usafirishaji hao wamewasha mwanga na
kuwa nuru kwenye jamii na kuwa pamoja na umuhimu wao huo baadhi ya watu wanaweza
kuwatumia vibaya kwa manufaa yao binafsi na kusahau maslahi mapana ya taifa
hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Alisema wanaweza kutumika katika vitendo vya kusafirisha
fedha za rushwa ambayo haina watu maalum wa kuitoa na kuipokea na kuwa
inawahusu watu wote wakiwemo viongozi na wataalam.
Machali aliwataka maafisa usafirishaji hao kuwa makini na
kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vyote vya rushwa kama ambavyo TAKUKURU
imekuwa ikiongoza kwenye mapambano hayo.
Alitaja Kauli mbiu ya TAKUKURU kuwa 'Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu' ambapo aliwaambia maafisa hao kuwa hawapaswi
kuona aibu ya kuitangaza kauli hiyo.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Petro Horombe awali
akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi alisema hivi sasa takwimu
zinaonesha watanzania tupo takribani milioni 68.56 kati yao asilimia 70 ya
watanzania hao wapo chini ya miaka 30 ambao ni vijana.
“Kama tumedhamiria kupambana na rushwa katika uchaguzi na
tungeliacha kundi ili la vijana tungefanya makosa makubwa ndiyo maana TAKUKURU Mkoa
wa Singida tukatambua umuhimu wao na kuandaa semina hii,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mkalama, Yassin Mohamed alisema zoezi la uchaguzi mkuu lipo kikatiba na hufanyika kwa kila mwananchi kumchagua Rais, wabunge na madiwani.
Alisema kwa upande wa Tanzania Bara, mchakato mzima
unasimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo inahakikisha kila
hatua inafanyika kwa uwazi, haki na usawa.
Kwa upande wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndiyo inayosimamia uchaguzi wa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. Hii inahakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi zote mbili.
Michael
Komba Mwenyekiti wa Usafirishaji wa Kijiji cha Kinyangiri akizungumza kwa niaba ya
wenzake aliishukuru TAKUKURU kwa kuwapa elimu hiyo ambayo inakwenda kuwasaidia kwenye mapambano dhidi ya rushwa na kuwa watawafikishia wenzao ambao
hawakupata fursa ya kuhudhuria semina hiyo.
“Tunaomba
semina za namna hii ziwe endelevu katika maeneo mengine ya wilaya yetu ili kila
afisa usafirishaji aielewe,” alisema Komba.
Wema
Ndomba ambaye ni Wakala wa Huduma za Fedha alisema elimu waliyoipata imewafumbua macho na
kuelezea kuwa wanakwenda kuwa makini na fedha chafu ambazo watazitilia mashaka
na kuchukua hatua ya kutoa taarifa TAKUKURU kupitia namba ya bure ya 113.
Katika
semina hiyo mada mbalimbali zilitolewa na wawezeshaji wabobezi ikiwepo ya
usalama Barabarani na vitendo vya jinai ambavyo vimekuwa vikifanywa na maafisa
usafirishaji hao kama vile ubakaji hasa wa wanafunzi, usafirishaji wa mali za wizi
na matumizi wa vyombo vya moto bila kufuata Sheria na taratibu mada iliyotolewa na Mkuu
wa Kituo cha Polisi Nduguti Mrakibu Msaidizi (ASP), Fedrick Magowa.
Aidha, ASP Magowa alitoa mada iliyohusu Mawakala wa Huduma za Fedha jinsi ambavyo wanaweza kuibiwa na watu wasiyo waaminifu na wao kujiingiza katika kutuma fedha za rushwa na utakatishaji wa fedha.
Mada
nyingine iliyotolewa ilihusu namna ya kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa
na Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu mada ambayo
ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka wilayani humo, Efrancia Nzota ambaye alieleza inatolewa bure na haina mianya yoyote ya rushwa.
Afisa wa TAKUKURU wa wilaya hiyo Jennifer Kyungai alitoa mada iliyohusu masuala mazima ya rushwa na makosa ya rushwa katika uchaguzi kama yalivyoainishwa katika sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge, madiwani na 1 ya mwaka 2024.
Mada hiyo ilijikita zaidi kukabiliana na vitendo vya rushwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika wiki ijayo.
Semina hiyo iliyoandaliwa na TAKUKURU katika wilaya hiyo imelenga kuongeza uelewa kuhusu uwajibikaji, uwazi na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa katika sekta ya usafirishaji (bodaboda) na kwa watoa huduma za kifedha hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Petro Horombe akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi.
Mgeni rasmi mkuu wa wilaya hiyo, Mhe. Moses Machali akisisitiza jambo katika semina hiyo. Kushoto ni Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Petro Horombe na kulia ni Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mkalama, Yassin Mohamed.
Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Mkalama, Yassin Mohamed, akizungumza kwenye semina hiyo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Nduguti Mrakibu Msaidizi (ASP), Fedrick Magowa, Naibu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Petro Horombe na mkuu wa wilaya hiyo, Mhe. Moses Machali.
Afisa wa TAKUKURU Wilaya ya Mkalama, Jennifer Kyungai akitoa mada kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Nduguti Mrakibu Msaidizi (ASP), Fedrick Magowa, akizungumza ba Maafisa Usafirishaji katika semina hiyo.Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka wilayani humo, Efrancia Nzota.akitoa mada kuhusu mikopo ya asilimia 10.

Semina ikiendelea. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Petro Horombe.
Maafisa Usafirishaji wakiwa kwenye semina hiyo
Semina ikiendelea.
Maafisa Usafirishaji wakiwa kwenye semina hiyo.
Maafisa Usafirishaji wakifuatilia mafunzo hayo.
Taswira ya mafunzo hayo.
Afisa Usafirishaji Omari Athumani akizungumza.
Wakala wa Utoaji Huduma za fedha, Mussa Maduhu akizungumza.
Afisa Usafirishaji Seleman Johnson akichangia jambo kwenye semia hiyo.
Mwenyekiti wa Usafirisha Kijiji cha Kinyangiri, Michael Komba akizungumza.
Afisa Usafirishaji Michael Emmanuel akizungumza.
Wakala wa Huduma za fedha, Wema Ndomba akizungumzia fursa walioipata kupitia semina hiyo.
Viongozi mbalimbali pamoja na mgeni rasmi (katikati mbele), wakiwa katika picha na baadhi ya maafisa usafirisha ambao waliwawakilisha wenzao.







0 Comments