USSI APOKELEWA KWA KISHINDO ZANZIBAR BAADA YA KUMALIZA MBIO ZA MWENGE

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ismail Ali Ussi akipokelewa Zanzibar.

.........................................

Na John Walter -Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ismail Ali Ussi, ambaye pia alikuwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, amepokelewa kwa shangwe na hamasa kubwa na vijana wa mkoa huo mara baada ya kumaliza rasmi majukumu ya kukimbiza mwenge.

Ussi, ambaye ametumia siku 227 akiongoza mbio hizo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, alipokelewa kwa gwaride la vijana, nyimbo za uzalendo na mabango ya kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa niaba ya vijana wa taifa.

Akizungumza baada ya mapokezi hayo, Ussi alisema kuwa uzoefu alioupata katika kipindi chote cha kukimbiza mwenge ni wa kipekee, kwani umemwezesha kuona namna Watanzania wanavyoendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya amani, umoja na uzalendo.

“Tumepita kila kona ya nchi, tumeona namna wananchi wanavyoshiriki katika kujiletea maendeleo kupitia miradi inayofadhiliwa na Serikali, mashirika na wadau mbalimbali. Vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda amani na kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali,” alisema Ussi.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote waliotoa ushirikiano katika safari ndefu ya mwenge wa uhuru mwaka 2025.

Viongozi wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja walisema wanajivunia kiongozi huyo kwa kupeperusha vizuri bendera ya vijana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, wakimtaja kuwa mfano bora wa uongozi wa kizalendo na wa kujituma.

Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 umekimbizwa katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na visiwani, ukiwa na kaulimbiu ya kuhamasisha umuhimu wa kudumisha amani, kuimarisha uchumi na kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments